Sunday, 18 May 2014

MUHTASARI WA KIKAO CHA KWANZA CHA KAMATI YA RASILIMALI NA UWEKEZAJI

Ndugu Wanajumaru na wadau wengine kwa ujumla napenda kuwaletea taarifa /muhtasari wa kikao cha uwekezaji na rasilimali - cha kamati iliyo chaguliwa kupitia JUMARU kilichofanyika
 tarehe 04. 05. 2015 Mtanzania Hotel – Tandale Uzuri Kinondoni kama ifuatavyo:

Agenda za Mkutano:
1.      Kufungua Mkutano
2.      Kuchagua Mwenyekiti wa Kamati
3.      Uendeshaji wa Kazi za Kamati
4.      Hadidu Rejea za Kamati – ToR
5.      Tafakari ya Taasisi ya JUMARU na Uwekezaji Mkoani Rukwa
6.      Safari ya Mkoani Rukwa Kufafanua Majukumu ya Wanakamati
7.      Utaratibu wa Mkutano utakaofuata
8.      Mengineyo kwa idhini ya Mwenyekiti
9.      Kuahirisha Mkutano
Agenda No. 1: Kufungua Mkutano
Kikao kilifunguliwa rasmi mnamo saa 12:03 jioni baada ya kumteua mjumbe mmoja aliyeongoza sala ya kumshukuru Mungu na kuomba ulinzi wake. Kwa kuwa kilikuwa ni kikao cha kwanza kabisa, wajumbe walimuomba Katibu Mkuu Jumaru aongoze majadiliano ya muda mfupi ili kuweza kupata Mwenyekiti wa Kamati wa kudumu.
Katibu wa Kamati Bwana Credo Simbeye
wengine waliohudhuria ni 
1.      Herman Clement Kapufi – Mwenyekiti (Mkuu wa wilaya ya Same )
2.      Jane B. Chambi – Makamu Mwenyekiti
3.      Credo N. Simbeye – Katibu wa Kamati
4.      Justine Sangu – Mjumbe
5.      Joachim B.A. Sikulumbwe – Mualikwa (Katibu Mkuu JUMARU)
6.      Didas P. Mfupe – Mshauri /Mualikwa
7.      Arcardo Nchinga – Mualikwa
Wasiohudhuria:
1.      Mrs. Sikazwe Helen – Kwa taarifa
2.      Ms. Agness Robert – Kwa taarifa
Agenda No. 2: Kuchagua Mwenyekiti wa Kamati.
Ufafanuzi ulitolewa kwamba Kamati hii itakuwa ndiyo muhimili mkuu wa mwelekeo wa malengo ya Jumaru. Sifa mojawapo ya kiongozi atakayechaguliwa ni
kuwa  na uwezo wa kuona mbali katika kutafakari masuala mbalimbali ya maendeleo, mwenye haiba na hasa ya uwezo wa  kushawishi umma wa watu ndani na nje ya vikao kwa kuwa yeye ndiye atakuwa taswira ya matarajio ya utendaji wa kamati. Awe pia ni mwenye uwezo wa kuongea na ngazi yoyoye ndani na nje ya nchi inapobidi kuelezea masuala ya JUMARU na uwekezaji. Baada ya ufafanuzi huo wajumbe walielewa vema na kuteua moja kwa moja jina la DC wa Same ndugu Herman Clement Kapufi kuwa Mwenyekiti wa Kamati. Katika kuangalia uwiano wa kijinsia, makamu mwenyekiti alipendekezwa na kukubaliwa Ms Jane B. Chambi ambaye pia ni Afisa Uhamiaji Mkoa wa Dar es salaam. Pamoja na Jane kusita kupokea wadhifa huo, wajumbe walimfafanulia kuwa wanaopewa majukumu ndani ya JUMARU wasiogope maana ni wakati wao wa kuandaliwa kuwa viongozi wa baadaye. Wajumbe wote kwa pamoja walilidhia uteuzi wa majina yote mawili na Mwenyekiti alikabidhiwa rasmi kiti.

Kwa kuwa pia kule Mkoani Rukwa kwa maana ya Sumbawanga ilikuwa ni lazima kuwepo uongozi baada ya uteuzi wa awali wa Katibu ndugu Ardius Kwimba, wajumbe walitumia fursa hii kumteua Makamu mwingine wa Mwenyekiti kwa niaba ya wajumbe wa kule ambaye ni ndugu Rainer F. Lukalah kusimamia masuala ya Kamati lakini kwa ushirikiano na Mwenyekiti ndugu Kapufi.

 Agenda No. 3: Uendeshaji wa Kazi za Kamati
Katika kikao hiki Mwenyekiti mteule alifafanua kwamba kuwepo uongozi wa Kamati Mkoani yaani Sumbawanga na hapa Dar es salaam haina maana ya kuwa na kamati mbili zenye majukumu tofauti. Kazi zote zitaongozwa na kusimamiwa na Mwenyekiti wa Kamati kama ilivyo katika utendaji wa kila mahali. Jambo la pili utendaji utaongozwa na hadidu rejea kama zilivyoainishwa na kisha kwa kila kikao ambacho kitafanyika ama mkoani au Dar es salaam kutakuwepo na mawasiliano ya maridhiano ya pande zote mbili juu ya maamuzi yanayokusudiwa na kupitishwa.

Mapendekezo mengine kutoka kwa wajumbe ilikuwa ni kuiomba kamati kuangalia uwezekano wa kuwa na majina mengine ya wajumbe nje ya yale yaliyoteuliwa ambao si lazima wahudhurie vikao bali kutokana na wanavyofahamika juu ya ukereketwa wao kwa maendeleo ya Mkoa wa Rukwa. Baadhi ya majina hayo ni pamoja na:-
Father Simchile (yuko Uholanzi), Mr Sikazwe (yuko Marekani), Father Lucas (yuko Ujerumani), Credo Sinyangwe, Luzango Pangani Mfupe ambaye ni mhadhiri Pretoria, South Africa, na wengineo. Zaidi ya hayo pia wajumbe walishauri kuwaendea wenye viwanda kama EPZ kupitia kwa ndugu Robert Massawe ambaye ni mmoja kati ya viongozi (Manager) ndani ya kampuni hiyo kuona uwezekano wa kuwa na kiwanda kule Mkoani Rukwa. EPZ wanashughulika na ‘garments’  au vitambaa.
Mbali na mapendekezo hayo pia wajumbe waliona vema kuongeza idadi ya wajumbe wa Dar es salaam hasa wale wanaofahamika kwa ajili ya moyo wao wa kujitoa kwa ajili ya Mkoa wa Rukwa. Pia waliona kufanya hivyo kutasaidia katika kufanya kazi kama secretariat. Majina ambayo yalipendekezwa kuingizwa kwenye kamati ni pamoja na:-
1.      Ms. Stella Mwanansao – Tanzania Investment Bank
2.      Ms. Zoe Kastiko – Manager NMB Magomeni
3.      Mr. Philbert Michese – Tanzania Telecommunications Company Limited – TTCL
4.      Ms. Macelina Kisanko – Tanzania Harbors Authority – THA

Agenda No. 4: Hadidu Rejea za Kamati – TOR
Katibu Mkuu wa JUMARU aliwakabidhi wajumbe wa Kamati ya Rasilimali na Uwezeshaji hadidu za Rejea ambazo ndiyo msingi na mwongozo wa kiutendaji wa Kamati. Alisema kuwa lengo la kukabidhi ni kutoa fursa kuzipitia kwa makini na kisha kama kuna nyongeza au marekebisho yawasilishwe kwake kwa lengo la kuziweka rasmi kwenye kumbukumbu. Aliongeza kuwa hiyo itafuatiwa pia rasmi na kukabidhiwa barua za uteuzi kwa kila mjumbe.

Agenda No. 5: Tafakari ya Taasisi ya JUMARU na Uwekazaji Mkoani Rukwa.
Katika kuhakikisha kuwa na fursa zisizo na utata kwa ajili ya wawekezaji, wajumbe waliona ingekuwa vema kuhakikisha kuwa yale maeneo ambayo kwa sasa yametolewa kwa JUMARU kutoka kwa wananchi pamoja na vijiji, yashughulikiwe kupata hati miliki za ardhi mapema. Katika upimaji huo wa ardhi itakuwa vema kama mkoa utashirikishwa ili kupunguza usumbufu unaotokana na desturi za urasimu katika utendaji.

Zaidi ya hayo wajumbe waliona na kushauri kwamba ingekuwa vema pia kuona  JUMARU kama Taasisi inakuwa na maeneo ambayo yenyewe itawekeza miradi mbalimbali iliyo ndani ya uwezo wake. Mifano ilitolewa kwamba katika suala la ujenzi wa chuo/vyuo mara nyingi si rahisi mwekezaji akawekeza kwenye miundo mbinu yote. Ni fursa nzuri kwa JUMARU kuona uwezekano wa kupata ardhi kwa ajili ya kujenga na kumiliki huduma kama za Hostels, cafeteria, stationaries nk. Ni rahisi sana kuingia katika ubia na taasisi au mifuko ya fedha kama vile NSSF, PPF na hata Bank kama hati miliki zikiwa sahihi. Jambo hili tunapolitafakari ni lazima liwe wazi hata kwa uongozi wa mkoa ili tunapoanza kutafuta hati milki iwe rahisi kupata nguvu.

Wakati jitihada zinabuniwa ni jinsi gani wawekezaji wanaweza kushirikiana na wananchi kuleta maendeleo mkoa wa Rukwa, wajumbe waliona ni vema kufuatilia taarifa za mkoa kuhusu fursa mbalimbali za kuwekeza kwa imani kwamba lazima mkoa una taarifa za namna hiyo. Kamati iliona ni jukumu lake kuhakikisha kwamba taarifa hizo zinapatikana ili iwe rahisi katika kuainisha maeneo hayo. Zaidi ya hayo wajumbe walitoa wito kwa wana- Rukwa wengine wenye ardhi ya kutosha kutafakari jinsi ambavyo wangeweza kuwekeza kupitia chombo hiki cha JUMARU.

Katika kutafakari namna ya kushirikisha wadau mbalimbali katika kongamano la October na kutimiza miaka 40 ya kuanzishwa mkoa wa Rukwa, ndugu Herman Kapufi alikuwa tayari amekwishaongea na Vodacom Foundation hata kabla ya kukabidhiwa majukumu kama mwenyekiti wa Kamati ya Rasilimali na Uwekezaji. Katika mazungumzo hayo ndugu Kapufi alikuwa ameuomba uongozi wa Vodacom kuangalia namna ambavyo wangeweza kuwezesha maadhimisho hayo hasa kwa kudhamini michezo ya mpira kwa wanawake na wanaume. Katika udhamini huo aliomba mkoa usaidiwe mipira 32 ikiwemo mipira 16 ya miguu na mipira 16 mikono kupitia JUMARU. Maombi hayo yalifika kwa Mkurugenzi wa Vodacom na kukubaliwa kuwa wako tayari. Katika kuweka uzito kwa jambo hili ushauri ulitolewa kuwa JUMARU ifanye mchanganuo wa mahitaji ya udhamini huo ikiwa ni pamoja na mfumo wa tuzo zitakavyokuwa na kisha barua iandikwe KUPELEKA Vodacom Foundation kupitia kwa Waziri Mkuu kwa anuani ifuatayo:-
Mkurugenzi Mtendaji
Vodacom Foundation, S. L. P 2369, Dar es Salaam.
Pia mawasiliano ya kawaida yanaweza kupitia kwa Mr. Salum Mwalimu mmoja kati ya watumishi wa Vodacom  kwa kupitia smwalim@vodacom.co.tz  ambapo ndiyo mazungumzo kuhusu ufadhili huo yalipoanzia kabla ya kufika kwa Mkurugeni.

Ndugu Kapufi pia aliongeza kusema kwamba mdau mmoja wa Maendeleo ndugu SABODO alikwishaonesha nia ya kusaidia kuchimba visima virefu vya maji katika mkoa kulingana na atakavyopewa maelekezo. Hata hivyo idadi ya visima hivyo ni 4 tu japo kuna uwezekano wa kumshawishi walau kila jimbo katika mkoa likapata kisima kimoja ikiwepo maeneo maalumu ya watu wengi kama itakavyopendekezwa.

Agenda No. 6: Safari ya Mkoani Rukwa Kufafanua Majukumu ya Wanakamati
Katika kufafanua agenda hii, Katibu Mkuu JUMARU alisema kwamba ni vema awepo mtu kutoka ndani ya Kamati aweze kufika Sumbawanga na kuitisha Mkutano ambao utalenga kufafanua juu ya majukumu mbalimbali ya Kamati. Wajumbe wa mkoani Rukwa wanapaswa kuelewa kwamba mambo yatakayokuwa yanafanywa ni ya pamoja na si vinginevyo.

Agenda No. 7: Utaratibu wa Mkutano Utakaofuata
Mwenyekiti akifafanua agenda hii alisema kwamba, atawasiliana na kila mmoja kwa simu ili kuona uwezekano wa kuongea na kila mmoja. Kikao hicho ndicho kitatafakari vema namna ya kuwapata wawekezaji ambapo baada ya kuwapata, majina yao yatapelekwa Kamati Kuu ya JUMARU ili mawasiliano yafanyike. Matarajio ya kikao hicho ni mwisho wa mwezi wa tano.

Mwenyekiti alitumia fursa hii kuupongeza uongozi hususan Mwenyekiti wa JUMARU Ms. Helena Khamsini kwa namna nzuri waliyofanya kipindi tarehe 5/5/2015 asubuhi TBC1

Kulikuwa pia mapendekezo ya namna ya kuendesha Kamati hii. Katibu Mkuu wa JUMARU alisema kwamba kwa kuwa moja ya vigezo vya nguvu ya Kamati ni pamoja na kuwa na mfuko, inawezekana ikawepo fursa ya watu kutaka kuchangia mfuko huo. Kwa ajili hiyo ushauri ulitolewa kwamba, Kamati iwe na account yake ambayo itaitwa JUMARU INVESTIMENT ACCOUNT. Ushauri huu ulipokelewa na kwamba taratibu zitazingatiwa.

Agenda No. 8: Mengineyo kwa Idhini ya Mwenyekiti
1.      Katibu Mkuu alishauri kuwa pale inapowezekana si vibaya vyombo vya habari vikatumika kuelezea masuala mazuri ya JUMARU na Uwekezaji Mkoa wa Rukwa.

2.      Alisema kuwa Jumatano au Alhamis yaani kati ya tarehe 7 na tarehe 8 mwezi wa 5 kulikuwa maandalizi ya kufanya mazungumzo na waandishi wa habari yaani press conference. Kwa ajili hiyo aliomba wajumbe wa kamati kuwezesha mazungumzo hayo. Wajumbe walilipokea na kuweza kuchangia kiasi cha shilingi za ki-Tanzania 240,000/=

Agenda No. 9: Kuahirisha Mkutano
Mkutano uliahirishwa na Mwenyekiti mnamo saa 3:08 usiku kwa kuwatakia wajumbe kila la heri na kwamba baada ya kukamilisha mawasiliano na wajumbe basi tarehe ya mkutano mwingine itatangazwa.  Sala maalumu ya kumshukuru Mungu na kuomba uliza wake ilihitimisha.

No comments:

Post a Comment

regnard