ABOUT US


1.UTANGULIZI

1.1NENO LA SHUKRANI

Awali ya yote, sekretarieti ya JUKWAA LA MAENDELEO MKOA WA RUKWA (JUMARU) tunapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetufanikisha kunshirikiana nanyi, Wazee wa Mkoa wa Rukwa, katika mchakato wa kuanzisha na kuendeleza jukwaa la Maendeleo katika mkoa wetu.

Pili, tunapenda kuwashukuru ninyi Wazee wa mkoa wa Rukwa, pamoja na wana Rukwa wote kwa ujumla wenu kwa kuunganisha nguvu zetu pamoja na kuwa tayari kushirikiana pamoja kwa ajili ya maslahi ya mkoa wetu wa Rukwa na Taifa la Tanzania kwa ujumla wake.

Pia, tunapenda kushukuru uongozi wa mkoa wa Rukwa kwa ujumla wake kwa jitihada mbalimbali ambazo uongozi wa mkoa umeendelea kuzifanya kwa ajili ya kuleta maendeleo ndani ya mkoa wetu. Haitakuwa rahisi kumshukuru kila mmoja kwa nafasi yake kama Mtanzania kwa namna alivyoshiriki na ambavyo ameendelea kushiriki katika kuchangia maendeleo ya mkoa wa Rukwa kwa hali na mali. Tunawashukuru wote, Watanzania hata raia wa nchi nyingine waishio Tanzania na walio nje ya nchi yetu ambao mmekuwa mkishiriki katika kuleta maendeleo ndani ya mkoa wa Rukwa.

1:2 CHIMBUKO LA KUANZISHWA KWA JUMARU

Wazo la kuanzishwa kwa JUMARU linatokana na historia ya Maendeleo ya Mkoa wa Rukwa kupitia Mipango na Programu mbalimbali za Maendeleo ya wana Rukwa ndani na nje ya Mkoa wa Rukwa. Baadhi ya hatua zilizochukuliwa na wana Rukwa zikiwemo kuanzishwa kwa asasi mbalimbali za maendeleo ndani ya mkoa wa Rukwa zimepelekea kuona haja ya kuwa na JUMARU.

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo katika taasisi ya The Foundation for Civil Society Tanzania, zilizoainishwa katika tovuti yao hadi kufikia mwezi June 2013, mkoa wa Rukwa una asasi zipatazo 108 zisizo za serikali, bila kujumuisha madhehebu au dini mbalimbali. Orodha imewekwa katika kiambatanisho namba 1.
Asasi nyingi zilizosajiriwa ndani ya mkoa wa Rukwa zimelenga kushughulikia maeneo kadhaa ya maendeleo ya wana Rukwa. Hata hivyo, bado kuna ukosefu wa uwepo wa asasi zitakazoweza kuangalia maeneo yote ya maisha ya wana Rukwa yakiwemo ya uchumi, elimu na jamii kwa ujumla wake. Pia kuna ukosefu wa chombo kinachoziunganisha asasi zote pamoja na wadau wengine wa maendeleo ili kuongeza ufanisi na kasi ya maendeleo ndani ya mkoa wa Rukwa.

Pia chimbuko la JUMARU linatokana na kuanzishwa kwa Mfuko wa Elimu ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, zaidi ya miaka 10 iliyopita, kulipelekea kuona haja ya kuwa na chombo kitakachounganisha wana Rukwa wote katika kujiletea maendelea kwa kushirikikiana na mamlaka za serikali, mashirika ya umma na taasisi nyingine binafsi (zisizo za serikali).
Pia wazo hili la kuanzishwa kwa JUMARU linatokana na maazimio ya kongamano la wanavyuo vikuu na wadau wa maendeleo wanaotokea Mkoa wa Rukwa wanaosoma na waliosoma vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi ya Tanzania, lililofanyika Dar es salaam, Mgulani, yapata miaka mitatu iliyopita.