Utangulizi
Awali ya yote, “ili mbegu iote haina budi kufa.” Ni usemi wa miaka mingi, kwa
sehemu, ukimaanisha kwamba ni lazima kujitoa ili kuweza kufikia maendeleo bora
zaidi.
Kwa muda mrefu sasa, wana Rukwa tumekuwa na
jitihada za pamoja katika harakati za kujiletea maendeleo. Hii inathibitishwa
na uwepo wa asasi nyingi zisizo za serikali, zilizoanzishwa na wana Rukwa
wenyewe ambazo kwa ujumla wake, zinalenga kuunga mkono jitihada za serikali
katika kuwaletea wana Rukwa maendeleo. Mpaka mwezi Julai 2013, kuna zaidi ya
Asasi zisizo za serikali zipatazo 110 ambazo zinafanya kazi ndani ya mkoa wa
Rukwa kwa malengo ya kushughulikia maeneo mbalimbali ya maendeleo ndani ya
mkoa. Huu ni ushahidi kuwa kwamba wana Rukwa tunayo shauku ya kuona maendeleo yanapatikana ndani ya mkoa
wetu.
Changamoto zinazotukabili wana Rukwa
Changamoto ni nyingi zinazotukabili, hasa kubwa ni
kiwango cha chini cha elimu; miundo mbinu duni (hasa upungufu wa barabara
zinazopitika katika majira yote ya mwaka); kilimo cha msimu kinachotegemea nvua
na kilichojikita katika mazao ya chakula. Kumekuwa na mkazo mdogo wa mazao ya
kudumu (hasa ya biashara) pamoja na ukosefu wa masoko mazuri ya mazao ya
kilimo. Zaidi sana mauzo ya mazao yetu yanafanyika pasipo kuyaongezea thamani,
jambo ambalo linapelekea kuuza mazao kwa bei ya chini. Pia yapo maeneo mengi ya
kiuchumi ambayo hayajaendelezwa ipasavyo kama vile utalii, madini, mazao ya
uvuvi,mifugo na mengine mengi yanayo hitaji jitihada za pamoja za wana Rukwa
katika kuyaendeleza.
Harakati za mabadiliko ya vichocheo vya maendeleo na uwekezaji ndani na
nje ya Rukwa
Mkoa wa Rukwa haujaachwa katika jitihada za
serikali ya Tanzania na Jumuia ya Afrika Mashariki (Jumuia) katika kuwaletea
wananchi wake maendeleo. Kwa mfano, tarehe 03 Mei 2006, Naibu Waziri, Wa Jumuia
ya Afrika Mashariki (wakati ule), Mheshimiwa Diodorus Buberwa Kamala, akitoa
mhadhara kuhusu mafanikio na changamoto za Jumuia katika chuo kikuu cha HULL,
nchini Uingereza, alieleza mojawapo ya mafanikio kuwa ni kuanzisha mchakato wa
kuimarisha mtandao wa barabara za lami zinazounganisha nchi wanachama wa Jumuia.
Katika mhadhara huo alisema miongoni mwa barabara zinazojengwa kutokana na
jitihada za pamoja za Jumuia ni pamoja na zile za Tunduma-Sumbawanga-Kasulu–Nyakanazi
(km 1,121) na Tunduma-Sumbawanga-Nyakanazi (km 1,056). Ujenzi wa
barabara hizi unalenga kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji kutoka
sehemu moja hata nyingine ndani ya eneo la “soko moja” (Common Market) ndani ya
Jumuia ya Afrika Mashariki. Kwa hiyo, Rukwa ni miongoni mwa sehemu nyeti zenye
fursa za kiuchumi kwa jumuia ya Afrika Mashariki.
Nchi za Afrika (kwa mujibu wa sera mpya ya mambo ya
nje ya Tanzania 2001, ukurasa wa 8) kwa msukumo wa Umoja wa Afrika, zipo katika
mchakato wa kuanzisha Jumuia ya Kiuchumi ya Afrika kufikia mwaka 2034. Jumuia
ya kiuchumi ya Afrika itafungua zaidi ushindani wa kibiashara na ongezeko la
fursa za uwekezaji.
Pia, repoti ya Wizara ya nishati na madini,mwaka 2013,
inaonyesha utafiti wa mafuta na gesi katika maeneo ya bonde la ufa ulianza
mwaka 2010 kwa kutoa leseni za utafutaji kwenye maeneo ya Ziwa Tanganyika Kusini,
Ziwa Rukwa, Bonde la Kyela, Malagarasi, Pangani, Ruhuru na Kilosa-Kilombero.
Utafutaji wa maeneo haya bado upo katika hatua za awali. Ni miaka 60 toka
utafutaji wa mafuta na gesi uanze miaka ya 1950 chini ya Kampuni za BP na
Shell.
Kwa sisi wana Rukwa mabadiliko haya ni makubwa na
ya maana sana kwetu kwa vile “yanatupigia kengele ya kutuamsha ili tusije
tukachelewa kuhesabu namba shuleni, tukaishia kula viboko vya mwalimu.”
Ni lazima wana Rukwa tukubali kutekeleza usemi wetu wa “Rukwa Ruka”, turuke badala ya kutembea mwendo wa kinyonga, katika
kushughulikia masuala yatakayoleta maendeleo mkoani, ili tupate kuwa ni sehemu
ya kunufaika na mabadiliko ya mazingira ya kiuchumi yanayoendelea nchini na
barani Afrika kwa ujumla wake. Vinginevyo, badala ya Rukwa Ruka tunawezakuishia
kwenye “Rukwa rukwa”.
Mabadiliko haya yana maana sana kwetu kama wana
Rukwa kwa vile “yanatupigia kengele ya kutuamsha ili tusije tukachelewa kuhesabu namba
shuleni, tukaishia kula viboko vya mwalimu.” Ni lazima wana Rukwa
tukubali kutekeleza usemi wetu wa “Rukwa
Ruka”, turuke badala ya kutembea mwendo wa kinyonga, katika kushughulikia
masuala yatakayoleta maendeleo mkoani, ili tupate kuwa ni sehemu ya kunufaika
na mabadiliko ya mazingira ya kiuchumi yanayoendelea nchini na barani Afrika
kwa ujumla wake. Vinginevyo, badala ya Rukwa Ruka tunawezakuishia kwenye “Rukwa rukwa”.
Nini kifanyike?
Ni
lazima tuanze na suala la ELIMU.
Tazama,
kwa mfano, idadi ya shule za msingi ndani ya mkoa ni 352 hadi 2012. Wakati huo
huo, shule za sekondari zipo 80 tu na kati ya hizo ni 10 tu ambazo zinatoa
elimu ya kidato cha sita. Hii inamaanisha kwamba sehemu kubwa ya vijana
wanaohitimu darasa la saba hawapati fursa ya kuendelea na masomo ya sekondari
na hata wanaopata nafasi ya kuendelea na sekondari kuna nafasi finyu za kuingia
kidato cha 5 &6. Matokeo yake, wengi watategemea kilimo, tena kwa sasa
kilimo cha mazao ya msimu, yanayochukua eneo kubwa la ardhi (kwa mfano
mahindi). Mwisho wa siku, hakutakuwa na ardhi ya kuwatosha baada ya miaka michache
ijayo. Hivyo basi, mkoa unakabiliwa na uwezekano wa kuzuka kwa migogoro ya
ardhi inayoweza kupelekea ukosefu wa amani na usalama ndani ya mkoa kwa siku za
usoni kwa vile sehemu kubwa ya wakazi, hasa vijana na watoto wa sasa, watakuwa
ni tegemezi kwa kilimo hali fursa nyingine za uwekezaji na ajira zinazohitaji
ushindani wa soko watakuwa hawana ‘ubavu’
wa kupigania! Tukumbuke kwamba mkoa unakabiliwa na ongezeko la kasi la idadi ya
watu, kutoka watu 730,050 (Mpanda ikiwemo) mwaka 1988 hadi kufikia watu
1,004,539 mwaka 2012 (bila Katavi). Tukitoa uwiano wa ongezeko la watu Katavi kutoka
mwaka 1988, tunapata ongezeko la idadi ya watu kwa asilimia 115 kwa mkoa wa
Rukwa pekee ndani ya miaka 24.
Tuungane katika yapi?
Mosi,
tushirikiane kuwezesha mazingira bora ya elimu ndani ya mkoa, kuanzia ngazi ya
shule za awali, msingi, sekondari, vyuo vya ufundi na elimu ya juu. Mazingira
bora ya elimu yanahusisha uwepo wa taasisi za elimu za kutosha, idadi sawia ya
walimu au wakufunzi, uwepo wa vifaa vya kutosha vya kutolea mafunzo na mengine
mengi. Kwa mfano, katika shule za msingi pekee tuna upungufu wa walimu 918 hadi
mwaka 2012. Sekondari hali kadharika, kuna upungufu mkubwa. Hivyo, basi nitoe
wito kwa vijana wenzangu na wana Rukwa kwa ujumla, tuone haja ya kukimbilia
kufanya kazi mkoa wa Rukwa ili kusaidia kupunguza pengo la walimu, hasa shule
za msingi.
Pili,
tuungane kuanzisha chuo kikuu ndani ya mkoa wa Rukwa, ama kupitia asasi za
maendeleo, taasisi za dini nakadharika – Chuo Kikuu kitasaidia kuongeza idadi
ya wataalamu na wanataaluma katika maeneo mengi na hivyo kuondoa upungufu wa
walimu, na wafanyakazi wa kada mbalimbali. Pia kitaongeza uwezekano wa kuwepo
tafiti zaidi katika kilimo ili kutuwezesha kuleta mapinduzi katika kilimo,
tukizingatia Rukwa na Kilimo ni kama samaki na maji.
Ndiyo,
tunafahamu kwamba kuna upungufu wa wanataaluma katika sehemu nyingi za nchi
yetu, lakini tukiwa na chuo kikuu ndani ya mkoa, tunahakika kwamba sehemu kubwa
ya wahitimu watapenda tu kubakia kufanya kazi ndani ya mkoa. Uanzishwaji wa chuo
kikuu unawezakwenda sambamba na ongezeko la shule na oboreshaji wa mazingira ya
utoaji elimu kuanzia ngazi ya chini. Wana Rukwa tusifikiri kwamba kwa serikali
kuwa na shule katika kila kata basi inatosha! Kata zetu zilizopo nyingi ni
kubwa sana! Tunaoweza kuwekeza katika shule na vyuo binafsi tuone kuna haja na
kuna pengo kubwa linalotudai tulijaze!! Maeneo yote ya utoaji wa elimu na
huduma kama vile afya, yanahitaji jitihada zetu kama wana Rukwa kwa umoja wetu
na jitihada za mwana Rukwa mmoja mmoja.
Tatu,
Asasi zote zinazofanya kazi ndani ya mkoa wa Rukwa, pamoja zione haja ya
kufanya kazi kwa kushirikiana zaidi. Kwa uelewa wangu, asasi zote zinalenga
kuhakikisha maendeleo yanapatikana ndani ya mkoa wa Rukwa kwa manufaa ya wana
Rukwa. Hivyo basi, ni wakati wa kuona namna ambavyo asasi za maendeleo zinaweza
kushirikiana ili kuunga mkono, kwa ufanisi, jitihada za serikali na zile za wadau
wengine wa maendeleo ndani ya mkoa wa Rukwa. Tukumbuke wahenga wetu walivyonena
masikioni mwetu “ Umoja ni nguvu, na
utengano ni udhaifu.” Hivyo basi, tusilale ama kusinzia, mpaka tuone mkoa wetu
una ruka.
Nne,
Wana Rukwa tuone haja ya kufanya uwekezaji utakaongeza thamani katika mazao na
hivyo kupelekea ongezeko la fursa za ajira. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia ni
kilimo ambacho kina uwezo wa kubadili maisha kwa kupunguza umaskini kwa kadiri
ya mara nne zaidi ya uwezo wa sekta nyingine yoyote ile duniani kwa sasa. Aidha
kwa taarifa hizo hizo za Benki ya Dunia ajira moja katika mchakato wa kuyapatia
mazao ya kilimo thamani huwezesha uundaji wa ajira tatu hadi nne katika nchi
maskini na hadi ajira mbili katika nchi zilizoendelea. Aina nyingi za mazao yazalishwayo mkoani Rukwa
yatawezesha ujenzi wa viwanda vingi vinavyoweza kutoa ajira kwa kiasi cha
kupunguza pengo la ukosefu wa ajira ndani ya mkoa na nchi yetu kwa ujumla.
Aidha mahala popote duniani kuliko na viwanda vya nafaka ndiko kunakozalishwa
mifugo kwa wingi kwa vile nafaka na mabaki/ mashudu ya nafaka yanayozalishwa
katika mchakato wa kuongeza thamani ya nafaka hutumika katika kulisha aina
nyingi ya mifugo kama kuku, ngombe, nguruwe na samaki.
Kutokana
na mifugo bidhaa za nyama, maziwa na ngozi huzalishwa. Ngozi nazo zaweza
kuzalisha viwanda vya bidhaa lukuki kama vile mabegi, nguo za ngozi, mikanda,
mikoba, pochi, vifunikizo vya samani majumbani na katika vyombo vya usafiri
kama magari
Hitimisho
Si
wakati wa kunyosheana vidole na kidole kimoja hakivunji chawa. Kila mwana Rukwa
aone ana fursa sawa na mwingine katika kuchangia maendeleo ya mkoa wetu na
taifa letu kwa ujumla. Tusimame, tuungane na tushikamane kwa bidii ya kazi za
mikono yetu, kila mmoja kwa uwezo na vipawa alivyopewa na mwenyezi Mungu, ili
tuinue mkoa wetu katika nyanja zote za maendeleo.
Mbegu
lazima ife ili iote. Hakuna wa kumnyoshea kidole, wewe na mimi lazima tuwe ni
mbegu, ili tuzae matunda. Kumbuka ubora wa mazao unategemea ubora wa mbegu
iliyopandwa! Lazima tujitoe kwa bidii zaidi, kwa ubora zaidi na kuungana kwa
gundi isiyoyeyuka kama si kwa kukaza umoja wetu kwa ‘bolti na nati’ za daraja, zisizopata kutu wala kulegea kwa
urahisi, ili kuleta maendeleo ndani ya mkoa wetu.
Kumbuka
katika vitabu vya Mungu imeandikwa “Asiye
wajali wa kwao ni mbaya kuliko mchawi.” Maneno haya yanatuhimiza kuangusha
na kuvunja chembe zote za ubinafsi linapokuja suala la kujikwamua katika
maendeleo.
Na Titus Solomon Simsamba (pichani)
Agosti 2013
ni kweli wanarukwa tunahitaji umoja,mshikamano,na uvumilivu hasa vijana wenye nguvu kwani umoja ni nguvu utengano ni udhaifu
ReplyDeleteTUNASHUKURU SANA KWA COMMENTS ZAKO ZINAZO ONESHA MOYO WA UZALENDO, KATIKA MKOA WETU WA RUKWA.
Delete