Sunday, 18 May 2014

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

 (PRESS CONFERENCE)
MKUTANO NA VYOMBO VYA HABARI
UKUMBI WA IDARA YA HABARI MAELEZO -DSM
TAREHE 14/05/2014 SAA 6:00 -7:00  MCHANA
Ndugu wanahabari,
Hamjambo wote.
Poleni na Hongereni kwa kazi.
Awali ya yote kwa niaba ya Jukwaa la Maendeleo Mkoa wa Rukwa (JUMARU), napenda kuwashukuru kwa kutoa muda wenu kuwepo hapa kutusikiliza.  Asante sana na karibuni.

Ndugu wanahabari,


Jukwaa la Maendeleo Mkoa wa Rukwa (JUMARU) ni Asasi ambayo ilianzishwa kimkakati mwaka 2009 (kama Forum) na  vijana wasomi na wadau wanarukwa na kisha kupata Baraka za baadhi ya wazee wa mji wa Sumbawanga chini ya usimamizi wa Chifu Ludovick Kinyonto mnamo mwezi  Mei, 2012 na baadaye kuzinduliwa rasmi na baraza la wazee wa Mkoa wa Rukwa, baada ya maboresho ya malengo na muundo wake, tarehe 02 Machi 2013 pale Kebby’s Hotel, Mwenge, Dar es Salaam.  JUMARU imesajiliwa rasmi Wizara ya Mambo ya ndani ya Nchi tarehe30/8/2013 kwa No. S.A.18941 kama Asasi na pia imesajiliwa Wizara ya Viwanda na Biashara (BRELA) tarehe 03/07/2013 kwa No:35723 kama kampuni (isiyogawana faida)-Jukwaa la Maendeleo Mkoa wa Rukwa Company Limited na kwa sasa tunaendelea na mchakato wa kujisajili Wizara ya Katiba na Sheria (RITA) kama  Bodi ya wadhamini.
Viongozi wa jukwaa la Maendeleo mkoani Rukwa (Katikati) ni Helena Khamisi Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo Mkoa wa Rukwa katika kikao na Waandishi wa Habari Posta.

Ndugu wanahabari,

Lengo kuu la kuanzisha taasisi hii ni kuunganisha nguvu za hali na mali za wanarukwa wa ndani na nje ya Mkoa na wadau wote wa maendeleo,
katika kuhamasisha na kuchangia jitihada za kuwezesha maendeleo ya kweli ya wakazi wa mkoa wa Rukwa yanapatikana, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kisiasa  na pia katika kukabili changamoto za kimaendeleo pamoja na mgawanyo mzuri, matumizi sahihi, kuhifadhi, kulinda na kuendeleza rasilimali na maliasili zilizopo na  kutafuta na kutumia vizuri fursa za kimaendeleo zilizopo na zinazotengenezwa na kutolewa na serikali yetu na uwepo wa Mkoa wetu mpakani na nchi jirani za nje na kuwaandaa wanarukwa kwa ushirikiano wa soko la Afrika Mashariki na masuala mengine ya kimataifa.  Yapo malengo mengine mengi mahususi ndani ya katiba yetu ambayo tutaendelea kuelezana kila tutakapopata nafasi ya kukutana nanyi siku za usoni.

Ndugu wanahabari,

Ni vizuri pia nikawaeleza kwa kifupi muundo wa uongozi wetu kwa mujibu wa katiba tuliyoisajili kama Asasi. JUMARU tuna ngazi na vyombo vya uongozi kama ifuatavyo; mkutano mkuu wa wanachama wote, Baraza la viongozi, wazee na wadhamini, Bodi ya JUMARU Taifa, sekretarieti Taifa, sekretarieti za matawi ya ndani ya mkoa, vijiji na maeneo ya uzalishaji ,na mikoani – makao makuu ya mkoa na nje ya nchi (kwa wanao wasiliana)
Mpaka sasa JUMARU tuna wanachama hai zaidi ya 200 waliolipia kiingilio na kutoa michango kuwezesha shughuli zetu.  Pia tuna viongozi na wawakilishi wa muda katika mikoa 13 na nchi 11 wanaoratibu agenda zetu kulingana na malengo.  Tumefanikiwa kuendesha makongamano makubwa mawili (Dsm na Sumbawanga) na kuwakutanisha wanarukwa zaidi ya 600 pamoja na vikao vya kukutana na  wadau wa maendeleo wa ndani na nje ya mkoa.
Kwa mwaka 2013 tulifanikiwa kujichangisha fedha za kujiimarisha  (UENEZI) zaidi milioni 20, japo tuna madeni ya uendeshaji yanayofikia sh. Milioni 8 . Aidha, JUMARU ni taasisi ambayo imejipa jukumu la kuhamasisha NGO’s zote ndani ya mkoa wa Rukwa katika kuongeza mtandao na ushirikiano ili kufikia malengo ya kila mmoja. Uanachama wa JUMARU ni wa wazi kwa mtanzania yeyote mwenye mapenzi mema na mkoa wa Rukwa, kikundi, kampuni, taasisi, mamlaka, NGO chini ya masharti ya katiba yetu.  Kiingilio ni sh. 10,000/= kwa mtu mmoja, sh. 1,000,000/= kwa taasisi, kampuni, NGO au kikundi cha watu na ada ya kila mwezi ni sh. 5,000/= kwa mwezi mmoja kwa kila  mtu na sh. 60,000/= kwa kampuni au kikundi.
JUMARU tayari tulishakwisha jitambulisha kwenye mamlaka za kiserikali ngazi ya mkoa, wilaya na Halmashauri ndani ya mkoa, ofisi ya waziri mkuu na pia kwenye uongozi wa juu wa madhehebu ya kidini ndani ya mkoa na wengine kuwaalika kwenye majumuiko yetu tunayoandaa ili kufikisha ujumbe na kuuza mikakati yetu.
Ndugu wanahabari,
Lengo kuu la kuomba kukutana nanyi siku hii ya leo, kwanza ni kuwajulisha hayo niliyoyasema hapo juu, na pili ni kuwaomba ninyi mtusaidie kuujulisha umma wa watanzania na wadau wote wa ndani na nje ya Tanzania kuwa mwaka huu 2014 mkoa wa Rukwa unatimiza miaka 40 tangu kuundwa na kuzinduliwa kwake July 1974.  Hivyo basi sisi wanarukwa tunandaa sherehe za maadhimisho ya miaka 40 ya mkoa, ambapo tutatumia nafasi hii kutafakari nia na madhumuni ya kuomba kuundwa kwa mkoa kwa wakati huo na tutatathmini maendeleo ya mkoa ndani ya miaka 40 kiuchumi,kijamii, kiutamaduni na kisiasa ,mafanikio na changamoto na tutajadili na kuweka mkakati kama wakazi wa mkoa, tuendeje kuelekea nusu karne ya mkoa na miongo mingine mingi zaidi ijayo, katika kuweka sawa rejea za mkoa kwa vizazi vijavyo.
Kimkoa, maadhimisho ya miaka 40 ya mkoa yanaandaliwa na kuratibiwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Rukwa sambamba na kongamano la uwekezaji katika ukanda wa ziwa Tanganyika ambapo vyote vinafanyika mjini Sumbawanga mwezi Oktoba 2014, kama tulivyojulishwa mwezi Desemba 2013 na Mh. Stella Manyanya (mb) mkuu wa mkoa wa Rukwa na kwa barua aliyotuandikia machi mwaka huu na kutupatia jukumu maalum la kufanya  ambalo tunaendelea kulitekeleza.
Ndugu wanahabari,
Napenda kuwataarifu kuwa baada ya kushauriana kwa kina na Mh. Mizengo Pinda (MB) kama mwanarukwa na katavi, Mh. Manyanya mkuu wa mkoa na wadau wengine muhimu, Baraza la uongozi la JUMARU Taifa kwenye kikao chake cha kawaida cha tarehe 3/5/2014 lilipitisha azimio la kufanyika Hafla au Jumuiko la wanarukwa waishio Dsm na mikoa jirani tarehe 22/6/2014 pamoja na kuwaita baadhi ya viongozi wa JUMARU na wawakilishi wa wazee wa Sumbawanga, serikali na wadau ili tuje tupate nafasi ya kukutana na wadau wanaopenda kuwekeza mkoani kwetu katika kuwajengea uelewa mzuri zaidi juu ya mazingira ya mkoa wanaopenda kuwekeza mkoani kwetu katika kuwahamasisha ili mwezi Oktoba wakubali kwenda kushiriki kwenye kongamano la uwekezaji Sumbawanga.  Pia sisi wenyewe siku hiyo tutaweza kutathmini maendeleo ya mkoa kwa miaka 40, kufanya sherehe za awali kwa wanarukwa walio nje ya mkoa na kuweka mkakati wa  namna ya kujiandaa kushiriki, kuchangia maandalizi ya maadhimisho yanayo ratibiwa na ofisi ya mkuu wa mkoa kwa ajili ya octoba na kongamano la uwekezaji Ukanda wa ziwa Tanganyika
Katika kujipanga, baraza la JUMARU liliidhinisha rasmi uteuzi wa wajumbe wa kuunda kamati ya kudumu ya JUMARU ya Rasilimali, maliasili na uwekezaji yenye wajumbe 13 toka ndani na nje ya mkoa ambayo itaongozwa na mwenyekiti wake Mh. Herman Immaculata Clement Kapufi (Mkuu wa Wilaya ya Same).  Kamati hii ndiyo itatuongoza kutafuta na kuhamasisha wawekezaji wengi kadiri inavyowezekana, wa kushiriki Hafla yetu tarehe 22/6/2014 na kwenda kwenye kongamano la uwekezaji la Oktoba,  Sumbawanga.
Pia kikao cha baraza kilipokea taarifa na kupitisha azimio la kuunda kamati ya kuandaa hafla ya tarehe 22/6/2014  ambayo ina wajumbe saba 7 ikiongozwa na Bw Deusdedit Kisisiwe, kwa Dsm na kwa kule Sumbawanga wazee washauri wa kamati hii wataongozwa na Chifu Ludovick Kinyonto. Kazi ya kamati hii ni kupendekeza tarehe ya hafla, kuandaa bajeti, kutengeneza khanga na vitenge vya maadhimisho ya miaka 40 ya mkoa, kutafuta fedha za kufanikisha shughuli nzima na kuisimamia kikamilifu.
Kikao cha baraza, pia kilipokea taarifa ya kamati ya JUMARU ya Elimu na mchakato wa kuanzisha chuo kikuu ndani ya mkoa wa Rukwa. Kamati hii inaongozwa na Prof. Athanas Kauzeni. Lengo kuu la kamati hii ni kusaidia mapinduzi ya kifikra ndani ya mkoa kwa kuwezesha, maboresho ya taasisi za elimu msingi,  sekondari, VETA na uwepo vyuo viku vingi ndani ya mkoa tunapoelekea kuadhimisha nusu karne ya mkoa wa Rukwa.
 JUMARU, kwa kuongozwa na kamati hii, tayari tumefanikiwa kushawishi uongozi wa wamiliki wa St. Joseph University hapa Tanzania, mwaka huu wanafungua tawi lao Sumbawanga baada ya JUMARU kufanya jitihada za kutafuta majengo ya kuanzia na Ardhi ya kujenga majengo yao ya kudumu. Wadau hao tumewapata kutokana na ushirikiano mzuri tuliopata toka kwa Mh. Mizengo Pinda (mb) – Waziri Mkuu wa Tanzania, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na Mshamu Askofu Damian Kyaruzi – Jimbo Katoliki Sumbawanga, aliyetupatia majengo ya kuanzia chuo kikuu. Lengo la JUMARU, katika jitihada hizi pia ni kutaka kupata uzoefu na kisha kupitia chuo hicho (affiliation) tuweze kuanzisha Rukwa University ndani ya miaka michache ijayo.
St. Joseph University wako tayari kuanza kutoa mafunzo mwaka huu mwezi Oktoba.  Matangazo ya kuanza kutuma maombi ya kujiunga na chuo hiki, yameshasambazwa mkoa mzima wa Rukwa na Katavi. Ni matumaini yetu kuwa tunapoadhimisha miaka 40 ya mkoa na kongamano la uwekezaji, jiwe la msingi la majengo ya Chuo Kikuu cha St. Joseph litawekwa.  Karibuni nyie pia  kushuhudia tukio hili.
Ndugu wanahabari,
   JUMARU ina wajibu na inanuia kujiimarisha kiuchumi kupitia kampuni yake, na vyombo vingine tunavyotarajia kuvianzisha kama vile SASCCOS na  taasisi za kutoa huduma mbalimbali.
Kikao cha baraza cha tarehe 3/5/2014 kiliagiza na kupitisha, kwa mwaka 2014 mkakati wa kutekeleza mambo makuu saba ambayo ni:-
(1) Kutafuta na kusajili wanachama na kufungua matawi mapya na kuimasrisha yaliyotayari ndani na nje ya mkoa.
(2) Kutafuta fedha walau milioni 200 au wadhamini / wafadhili kuwezesha mipango ya mwaka 2014 na kulipia huduma za mwaka 2013.
(3) Kuandaa na kuendesha Hafla/Jumuiko la wanarukwa Dsm na mikoa jirani katika kuadhimisha miaka 40 ya mkoa na kuhamasisha wawekezaji wa kwenda kuwekeza mkoa Rukwa.
(4) Kuunda kamati ya Rasilimali, maliasili na uwekezaji chini ya JUMARU na kuipa hadidu rejea na kufanya tathmini, kupima na kupata umiliki wa kisheria wa ardhi tuliyopewa Sumbawanga
(5) Kusukuma agenda ya mchakato wa chuo kikuu kwa kushirikiana na St. Joseph University.
(6) Kuboresha katiba yetu na kuongozwa nayo katika utendaji wetu.
(7) Kuendelea kutekeleza maazimio ya kongamano la wanarukwa la Desemba, 2013 Sumbawanga.
Adhima yetu ni kuwa na mwanarukwa bora kielimu na kiuchumi, mwenye uwezo mkubwa wa kutambua, kutumia na kumiliki fursa za kiuchumi zinazomzunguka na zitakazojitokeza wakati wote na kuwa mlinzi na mhifadhi mazingira, rasilimali na maliasili za ndani ya mkoa kwa matumizi yake na urithi wa vizazi vijavyo.
Ndugu wanahabari,
Mwisho, baada ya kusema haya yote;
a)    nawaomba mtusaidie, kupitia taaluma yenu, kufikisha taarifa hizi kwa umma ili ushiriki katika yote tuliyopanga uwe wa mafanikio.
b)    nawakaribisha mshiriki nasi kwenye hafla yetu ya tarehe 22/6/2014 ya kujipanga kwa maandalizi ya maadhimisho ya miaka 40 na kongamano la uwekezaji yatakayofanyika rasmi Oktoba mwaka huu katika mji wa Sumbawanga chini ya usimamizi wa ofisi ya mkuu wa mkoa.
c)     mtusaidie kutangaza ili tupate wadau wenye moyo wa ukarimu na uzalendo wa kufadhili na kudhamini sehemu ya bajeti yetu kwa maandalizi ya shughuli hii kubwa na kumuunga mkono mkuu wetu wa mkoa wa Rukwa Mh. Eng. Stella Mamyanya (MB), kwa hali na mali, ili kufanikisha tukio hili muhimu sana mkoani Rukwa.
Natoa wito kwa wanarukwa wote popote walipo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwa mkoa wetu, tuungane kwa dhati ili tuuletee mkoa wa Rukwa maendeleo yanayotamaniwa na kuhitajiwa na wananchi wote wa mkoa huo.
Naomba sasa nitoe nafasi kwa wasaidizi wangu Mzee Paul Kimiti atoe historia ya mkoa wa Rukwa kwa kifupi tulikotoka, tulipo na tunakotaka kwenda. Naye Prof. Athanas Kauzeni awaeleze kwa nini msisitizo wa  Chuo Kikuu na mikakati iliyopo.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.
  “JUMARU, kwa Rukwa endelevu.  Pamoja tunaweza”
Bibi Helena Khamsini
Mwenyekiti wa JUMARU Taifa.









No comments:

Post a Comment

regnard