Tuesday, 31 December 2013

RUKWA WAASWA KUONGEZA JUHUDI KUJILETEA MAENDELEO

fuatilia makala iliyo andikwa na Mwenyekiti wa waandishi wa habari mkoa waRukwa Bwana Peti Siyame katika gazeti la tarehe 30/12/2013.

 "TAKWIMU za uchumi za mwaka 2011 zinaonesha kuwa sehemu kubwa ya wakazi wa mkoa wa Rukwa wanaishi katika dimbwi la umasikini, ambapo mkoa uliweza kuchangia asilimia 3 tu ya pato la Taifa.
“Mchango huu mdogo katika pato la taifa unaonesha maeneo mengi wananchi wa Rukwa wanatakiwa kuyafanyia kazi ili kuongeza mchango katika pato la taifa na wakati huo huo kuinua maisha ya wana Rukwa kiuchumi,” anabainisha Arkadius Kwimba ambaye ni Katibu Mkuu Msaidizi wa Jukwaa la Maendeleo Mkoa wa Rukwa (JUMARU).
Mwandishi wa makala haya hivi karibuni alipata fursa ya kuhudhuria kongomano la maendeleo lililofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Maurus mjini Sumbawanga lililoratibiwa na Jumaru na kuweza kufanya mahojiano maalumu na baadhi ya viongozi waandamiazi wa Jumaru.
Kwimba anatumia fursa hii na kueleza malengo ya Jumaru kuwa ni kuwaunganisha wana – Rukwa wote katika kuhamasisha na kuendeleza jitihada za kuleta maendeleo yao wenye ndani ya mkoa. Jumaru inalenga kuwa kiunganishi cha wananchi wa Rukwa wote, wanaoishi ndani na nje ya mkoa huu pamoja na asasi mbalimbali zinazofanya kazi ndani na nje ya mkoa huu.
Baadhi ya watoto walemavu na wasio walemavu kutoka mikoa ya Katavi na Rukwa wakishiriki mjadala wa ‘Fursa za Elimu ni Sawa kwa Watoto wote Tanzania’ uliofanyika mjini Sumbawanga mkoani Rukwa. (Picha na Peti Siyame).

Uwepo wa Jumaru utachangia kwa kiasi kikubwa katika kuunganisha nguvu za pamoja kwa wana – Rukwa, kuchochea kasi ya kuleta maendeleo endelevu ndani ya mkoa wetu huu,” anabainisha Kwimba.
Anaongeza kuwa
Jumaru kama jukwaa linatambua Serikali kama mshiriki nambari wani wa kusukuma mbele maendeleo ya Wana – Rukwa ambao licha ya miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula nchini kwa wingi bado wanaishi katika lindi la umaskini hivyo unatakiwa kujipanga vema ili kuongeza uzalishaji wenye tija.
Ili kupatia ahueni kiuchumi mwana-Rukwa ambaye ni mzalishaji wa mazao ya chakula kwa wingi nchini hivyo basi sasa ni lazima kama mkoa kuongeza uzalishaji si katika kilimo tu bali pia katika uvuvi na kuboresha ufugaji ili aweze kunufaika na furasa za soko huru la Afrika Mashariki.
“Hivyo basi Jumaru itakuwa na mchango mkubwa katika baadhi ya maeneo ikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji ……. chukulia kwa mfano mkoa huu (Rukwa) na jirani zetu wa Nyanda za Juu Kusini ambao ni mzalishaji mkubwa wa zao la mahindi, mathalani, hakuna uwekezaji wa kutosha katika kuongeza thamani ya mahindi yanayozalishwa.
Anasema kuwa kupitia Jumaru itamsaidia mwana – Rukwa kuibua fursa za uwekezaji katika kuongeza thamani ya mazao ya kilimo kabla ya kuyauza pia kuongeza thamani katika mazao husababisha kuongezeka kwa fursa za ajira. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia ni kilimo ambacho kina uwezo wa kubadili maisha kwa kupunguza umasikini mara nne zaidi ya uwezo wa sekta nyingine yoyote ile duniani kwa sasa.
Isitoshe kwa taarifa hizo kutoka katika benki hiyo ya dunia ajira moja katika mchakato wa kuyapatia mazao ya kilimo thamani huwezesha uundaji wa ajira tatu hadi nne katika nchi masikini na hadi ajira mbili katika nchi zinazoendelea. Anasema umaskini wa wakazi wa Rukwa unachangiwa kwa kiasi kikubwa na uwezo hafifu wa kuuza wanachozalisha hivyo kuwa na uwezo hafifu wa kununua kwa upande mwingine.
“Kuuza alichonacho mtu kwahitaji maarifa ya kuuza, maarifa ambayo yatatolewa kupitia kozi za muda mfupi na muda mrefu zitakazotolewa na Chuo Kikuu Rukwa kinachotarajiwa kujengwa na Jumaru,” anabainisha.
Kwa ujenzi wa chuo hicho kikuu mkoani hapa kutasaidia wafanya biashara na wadau wengine katika kilimo kupata maarifa ya kuwawezesha kutafuta masoko ya mazao au bidhaa za kilimo, uvuvi na ufugaji tofauti na sasa ambapo wengi wanauza mazao yao kwa walanguzi kwa bei ya kutupa.
“Isitoshe Mkoa huu una fursa kubwa ya uwezekano wa kuzalisha samaki (hybrid) wasioweza kuathiri samaki asilia katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa ambayo itawezesha ujenzi wa viwanda vingi vinavyoweza kutoa ajira kwa kiasi kikubwa hivyo kupunguza pengo lililopo la ukosefu wa ajira ndani ya mkoa wetu na nchi yetu pia,” anasema .
Mahala popote duniani kuliko na viwanda vya nafaka ndiko kunakozalishwa mifugo kwa wingi, ikiwemo nafaka na mabaki au mashudu ya nafaka yanayozalishwa katika mchakato wa kuongeza thamani ya nafaka hutumika katika kulisha aina nyingine ya mifugo ikiwemo kuku, ng’ombe, nguruwe na samaki.
Ngozi nazo zaweza kuzalisha viwanda vya bidhaa lukuki kama vile mabegi, nguo za ngozi, mikanda, mikoba, pochi, vifunikizo vya samani majumbani na katika vyombo vya kusafiria ikiwemo magari.
Kwa fasihi hiyo Katibu Mkuu wa Jumaru, Joachim Anatory anabainisha kuwa jukwaa hilo litatoa mchango mkubwa katika kuhamasisha wadau katika uwekezaji katika kilimo na mazao mengine ya kilimo “Lakini pia kupitia kampuni yake, Jumaru itakuwa ni mdau muhimu katika kuwezesha utekelezaji wa baadhi ya fursa za uwekezaji zilizopo ndani ya mkoa wetu huu,” anasisitiza Anatory.
Nasema kuwa ni matarajio ya Jumaru kwamba uwepo na ustawi wake utasaidia sana kuunga jitihada za Serikali na wadau wengine wa maendeleo mkoani Rukwa katika kupiga vita maadui watatu wanaolikabili Taifa letu, ujinga umaskini na maradhi.
“Sote Wana- Rukwa kwa pamoja na wadau wengine wa maendeleo, hatuna budi kuungana pamoja ili kuleta maendeleo katika mkoa wetu huu tunaamini kuwa hakuna mwingine atakayeinua hadhi ya mkoa wetu katika maendeleo zaidi ya jitihada zetu wenywe, tukiungwa mkono na wadau wa maendeleo ilhali tukishirikiana na serikali tunaamini pia kwa Rukwa endelevu Pamoja Tunaweza,” anafafanua .
Anaongeza kuwa Jumaru inaona kuwa Chuo Kikuu Rukwa kitakachoanzishwa kiendane na asili ya mazingira ya mkoa wa Rukwa na mikoa ya jirani ya Katavi na Kigoma ambapo anaorodhesha baadhi ya manufaa ya kuanzishwa kwake ikiwemo kuongeza utafiti wa mazao mbadala wa kilimo ikiwemo mazao ya biashara na kuwekeza katika kilimo chja kisasa.

Manufaa mengine ni pamoja na kuleta mapinduzi makubwa ya uvuvi katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Rukwa pia ongezeko la idadi ya walimu shuleni na katika vyuo utasababisha kupunguza upungufu mkubwa uliopo kwa sasa.

No comments:

Post a Comment

regnard