Saturday, 1 February 2014

Taarifa ya Kongamano la Maendeleo Mkoa wa Rukwa

  
TAARIFA YA KONGAMANO LA MAENDELEO MKOA WA RUKWA LILILOFANYIKA TAREHE 20 HADI 21 DESEMBA 2013 KATIKA UKUMBI WA CHEMCHEM – MJINI SUMBAWANGA: 

Utangulizi

Bodi ya JUMARU, Wadhamini na viongozi wa JUMARU taifa kwenye kikao chake cha tarehe 14 Jukai 2013 waliazimia na kuagiza kwamba JUMARU iandae matukio ya kuwaleta pamoja Wanarukwa na Wana-Katavi walioko ndani na nje ya mikoa katika mwezi wa Septemba 2013 (Dar es Salaam), na Desemba 2013 (Sumbawanga) na Marchi 2014(Dar es Salaam).

Malengo ya kuwakutanisha Wanarukwa na Wanakatavi yanatokana na historia yetu kwamba tumekuwa ni mkoa mmoja kwa miaka mingi. Hivyo basi, pamoja na kugawa mikoa, bado sisi ni jamii tunayoweza kushirikiana katika masuala mengi yanayohusu maendeleo yetu. Kukutana pamoja kunalenga kutupatia nafasi ya kujadili na kuona namna tunavyoweza kuchangia jitihada za Serikali katika kukabiliana na changamoto za maendeleo ya mikoa yetu na wananchi wake.

Hadi kufikia sasa tayari tumefanikiwa kuendesha kongamano Dar Es Salaam mnamo tarehe 01 Septemba 2013, lililofanyika katika ukumbi wa Urafiki Social Hall-Ubungo. Kongamano hili lilihudhuriwa na Wanarukwa na Wanakatavi wapatao 150 hali likigharimu kiasi cha TZS 5,350,000. Fedha zilizowezesha kufanyika kwa kongamano hili zilitokana na michango ya wanachama waanzilishi wa JUMARU.

·        Katika kongamano hili washiriki waliona haja ya uanzishaji wa vyuo vikuu katika eneo la maziwa makuu (Mikoa ya Rukwa na Katavi) kama sehemu ya kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za Kielimu, kilimo na maeneo mengine ya kiuchumi na kijamii. Katika kongamano hili, Jumla ya TZS 16,000,000 zilitolewa kama ahadi kwa malengo ya kuchangia mchakato wa kuanzisha chuo kikuu ndani ya mkoa wa Rukwa.

Kongamano la Sumbawanga

Tarehe 20 hadi 21 Desemba 2013 tulifanikiwa kuandaa na kuendesha kongamano Sumbawanga mjini katika ukumbi wa St. Maurus Chemchem. Kongamano lilipangwa kuwa la siku tatu lakini  lilifanyika kwa siku mbili likijumuisha idadi ya washiriki wapatao 400. Idadi kubwa ya washiriki walikuwa ni wakazi wa ndani ya Manispaa ya Sumbawanga, Sumbwanga vijijini, Kalambo na Nkansi.

    
SIKU YA KWANZA
Neno la Ukaribisho
          i.      Baada ya kupata taarifa kwamba usingeweza kufika katika siku ya kwanza kutokana na majukumu ya Kitaifa; Uongozi wa JUMARU taifa ulimwomba Dkt Chrisant Mzindakaya kutoa neno la ukaribisho kwa washiriki wa kongamano hali tukisubiri ufunguzi rasmi kwa siku ya pili. Katika maneno ya ukaribisho Dkt Mzindakaya alisisitiza yafuatayo:

           ii.        Umoja, mshikamano na upendo wa dhati  miongoni mwa Wanarukwa wote wa ndani na nje ya Mkoa ili kukabili changamoto za maendeleo;

          iii.        Wanarukwa kujenda utamaduni wa kurudi nyumbani kila mwaka wakiwa hai ili kujumuika na ndugu na jamaa zao badala ya kurudi wakiwa kwenye majeneza;

          iv.        kila Mwanarukwa ajenge nyumba ndani ya mkoa ili kuchangia maendeleo. Katika hili alisema yeye ni mzalendo wa mkoa na ili kuthibitisha hili hajawahi kujenga hata chumba cha msalani nje ya mkoa wa Rukwa;

           v.        Elimu itolewe kwa Wanarukwa hasa vijijini wasiuze ardhi/mapori na kiholela, tena kwa bei za kutupwa. Alisema mahali popote duniani, maendeleo huja kwa kutumia ardhi iliyopo siyo kutapanya ardhi kwa sababu zisizo za msingi;

          vi.        Hali ya wanasiasa kuanza kununua uongozi inatishaia mstakabali wa Mkoa na Taifa na tatizo la baadhi ya watawala/viongozi kukwaza jitihada za wawekezaji wazawa/wazalendo inakatisha tamaa;

         vii.        Yeye binafsi atakuwa tayari kutetea JUMARU na kusaidia lolote lililo ndani ya uwezo wake na kutumiwa popote katika jitihada za JUMARU kwa maendeleo ya Mkoa.
Baada ya Neno la ukaribisho kutoka kwa Dkt Mzindakaya, mada zifuatazo ziliwasilishwa:
     i.        Dhana ya JUMARU;
    ii.        Maendeleo ya elimu na mchakato wa kuanzisha Chuo Kikuu ndani ya Mkoa wa Rukwa; na
  iii.        Kilimo katika karne ya ishirini na moja na changamoto zake kwa tafsiri katika maendeleo ya mkoa wa Rukwa na ukanda wa maziwa makuu.
Wanakongamano walipata  nafasi ya kujadili mada azote katika siku ya pili


SIKU YA PILI

Ufunguzi wa kongamano

Ufunguzi wa kongamano ulifanywa kwa niaba yako na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Eng.Stella Manyanya(MB) katika siku ya pili
Katika hotuba ya ufunguzi, Mkuu wa Mkoa alitoa salamu zako kwa washiriki wa Kongamano na kueleza sababu za kutoshiriki kwako. Hotuba ya mgeni rasmi ilipokelewa vizuri sana. Baadhi ya masuala muhimu katika hotuba ya Mkuu wa Mkoa yalikuwa kama ifuatavyo:
     i.        JUMARU kuamsha na kuendeleza mshikamano wa dhati ndani ya mkoa kwa kufanya kazi inayozingatia malengo ya uanzishwaji wake. JUMARU kujiepusha kabisa katika kubeba ushabiki wa kisiasa la sivyo itakufa mapema;

    ii.        JUMARU kusaidia kukabili changamoto za maendeleo ya mkoa kwa ujumla hasa elimu na kushiriki utekelezaji wa maazimio mbalimbali ya maendeleo ndani ya mkoa kama vile Azimio la Kasense;

  iii.      JUMARU kusaidia kufufuaAsasi zilizolala kama vile UMARU, Mfuko wa Elimu wa kmbukumbu ya Mwalimu Nyerere na nyingine nyingi. Alisisitiza kwamba anapenda kuona Asasi zote zikifanya kazi kwa ushindani ili kuleta tija katika maendeleo ya Mkoa;

   iv.        Wanarukwa kujiunga katika vikundi vya kuweka na kukopa, ili kujipatia mitaji kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo;

    v.        JUMARU isaidie kueneza elimu ya kupiga vita maambukizi mapya ya VVU na kuhamasisha wanarukwa kupima afya zao ili kwa walioathirika waanze kupata dozi mapema;

   vi.        Alisisitiza juu ya kuendelea na jitihada za kukabili tatizo la watoto yatima na walio kwenye mazingira hatarishi ndani ya mkoa. Hata hivyo, aliweka wazi kwamba taarifa iliyokuwa imetolewa katika gazeti la Mwananchi kuhusu kuzagaa kwa watoto yatima ndani ya manispaa ya Sumbawanga lilikuwa limekuzwa kupita kiasi japo tatizo lipo; na

 vii.        JUMARU kuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na ofisi ya Mkuu wa Mkoa na mamlaka zake na kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa ujumla ili uwepo ufanisi katika kuleta maendeleo. 
     i.  

MAAAZIMIO YA KONGAMANO
Maazimio yafuatayo yalifikiwa :-
     i.        Wanarukwa kuungana kupitia JUMARU katika kujiletea maendeleo ndani ya mkoa wa Rukwa,
   ii.         Mchakato wa Chuo Kikuu Rukwa uendelee ;
  iii.        Elimu juu ya umiliki wa Ardhi kisheria ,matumizi bora ya na kutouza Ardhi itolewe
kwa wanarukwa
  iv.        JUMARU kuhamasisha Wanarukwa kuendelea kuwekeza ndani ya mkoa wa Rukwa ili kuleta
 maendeleo ifikapo juni 2019
    v.        JUMARU kuhamasi sha wanarukwa wanoishi nje ya mkoa na nje ya nchi kuwa na tabia ya
kurudi nyumbani Rukwa mara kwa mara
  vi.        JUMARU kuasidia kuibua na kuviendeleza vipaji vya watoto ndani ya mkoa wa Rukwa
 vii.        JUMARU kuwa na mawasilikiano mzuri na ofisi ya Mkuu wa Mkoa
viii.        JUMARU ihakikishe taasisi zilizopo na zilizokufa ndani ya mkoa zinafufuriwa na Zinaimarishwa
 mfano UMARU,Rukwa Community Bank na mfuko wa Mwalimu Nyerere




Kuhitimisha Kongamano
Mwenyekiti wa JUMARU (H Khamsini) aliahirisha Kongamano kwa kutoa shukrani za dhati kwa ushiriki wa Waziri Mkuu, kupitia Mkuu wa Mkoa wa Rukwa. Pia aliwashukuru washiriki wote wa Kongamano waliohudhuria na waliochangia kufanikisha kongamano. Pia aliishukuru familia ya Mzee Twende kwa moyo wa uzalendo waliouonyesha. Kongamano liliahirishwa mnano saa kumi na moja jioni.
Mafanikio ya kongamano

     i.        Kongamano la Sumbawanga, pamoja na kukabiliana na changamoto tulizozitaja, lilikuwa na mafanikio makubwa sana, kama ifuatavyo:

    ii.        Mwitikio wa watu ulikuwa ni mzuri sana na hasa baada ya kupata uthibitisho wa ushiriki wako kwenye kongamano. Michango ya mawazo iliyotolewa wakati wa kongamano inaonyesha dhamira ya dhati ndani ya watu ya kutaka kujiletea maendeleo. Tunapenda tukutaarifu kwamba taarifa za ushiriki wako katika kongamano zilipokelewa kwa hamu kubwa na upendo mkuu ndani ya mioyo ya watu


  iii.         Lengo kuu la kongamano la Sumbawanga ilikuwa ni kutangaza dhana ya JUMARU na kuwaleta pamoja Wanarukwa kwa malengo ya kujadili changamoto za maendeleo na kuhamasisha kuunganisha nguvu katika utatuzi wa changamato zilizopo. Mada zote zilizopangwa kuwasilishwa na kujadiliwa zilifanyika.

   iv.         Ushiriki - Tulipanga kuita washiriki 1, 000 wa ndani na nje ya mkoa ambapo tulifanikiwa kupata uwakilishi wa kutosha kwa kuanzia. Katika makundi tuliyoyaalika tulipata Mkuu wa Wilaya mmoja (Kalambo), Katibu wa Mbunge mmoja, Wenyeviti wa vijiji kumi na saba, viongozi wa dini-3, viongozi wa vyama vya siasa watano, Madiwani watano, Asasi kumi na tatu, taasisi za umma-SIDO, NMB, NBC, TPB, vyama vya wanataaluma(TAHOSSA-mkoa na TAMONGSCO) na wananchi wa kawaida na wawakilishi wa wanarukwa toka mikoani. Baadhi ya mikoa iliyotuma wawakilishi ni pamoja na Iringa, Ruvuma, Mbeya, Singida, Mtwara, Dar es Salaam, Katavi na Morogoro. Pia tulipokea salamu kutoka mikoa ya Kigoma, Tabora, Mwanza, Simiyu,  Dodoma, Arusha, Kilimanjaro, Pwani na Tanga ambao walipata dharura na kuchelewa siku rasmi za kongamano hasa kwa vikwazo vya ruhusa za kikazi na hali ya usafiri.

    v.        Familia ya Mzee Twende Nyakasi wa kijiji cha Pito, baada ya kuguswa na jitihada za JUMARU katika elimu imeamua kutoa eneo la Ardhi ya familia ekari Arobaini(40) kwa ajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Rukwa.

   vi.        Sambamba na hilo asasi ya KAESO ilitoa mchango wa kusaidia chumba cha ofisi katika jengo lake kwa ajili ya uongozi wa JUMARU Taifa. Pia KAESO walitoa miti ya mbao ya thamani ya Shilingi milioni moja kwa ajili ya kutumika pindi ujenzi wa Chuo Kikuu utakapoanza.

Imeandaliwa na Sekretariati- JUMARU.
                                                           
JUMARU: “KWA RUKWA ENDELEVU, PAMOJA TUNAWEZA”

No comments:

Post a Comment

regnard