Wednesday, 17 February 2016

NI KWELI WAHASTAHILI PONGEZI WABUNGE WALIOITUMIKIA MIKOA YETU KWA KIPINDI CHA MWAKA 2000 – 2015 PAMOJA NA WAKUU WA WILAYA, WAKURUGENZI WA HLMASHAURI NA MADIWANI WOTE?



Kwa namna ya kipekee kabisa JUMARU tunaomba tutumie fursa hii mbele ya watanzania wote kutoa pongezi na shukrani maalumu kwa viongozi wetu wote ambao walipata nafasi ya kuutumikia mkoa wa Rukwa wa zamani na baadaye mikoa ya Rukwa na Katavi ndani ya kipindi cha 2000 – 2015, wa kuchaguliwa (yaani wabunge na madiwani wote) na wale wa kuteuliwa na rais (yaani wakuu wa mikoa, makatibu tawala wa mikoa, wakurugenzi wa Halmashauri) na wakuu wa idara wote katika ngazi ya mkoa, Wilaya na Halmashauri pamoja na watumishi wote kwa ujumla,kwa kuwezesha mikoa yetu kuendelea kusonga mbele vyema  katika Nyanja zote za kimaendeleo na kiuchumi, kiutamaduni, kijamii na kisisasa.
Lengo langu la kutoa makala hii kwa wasomaji, kwa niaba ya jumuiya nzima ya wanarukwa na katavi ni kutaka kutoa pongezi maalum kwa wabunge wetu wote na madiwani wao ambao wamekuwa wasimamizi na wahamasishaji wakuu wa shughuli za maendeleo yetu. Hongeleni sana.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba katika kipindi hiki cha miaka 15  yaani 200 - 2015 mikoa yetu imepiga hatua kubwa za kimaendeleo katika maeneo mengi ambayo huko nyuma hayakutegemewa  kufikia hatua tulipo sasa, hasa kwenye miundombinu za barabara za lami na hata za changarawe zinazo pitika wakati wote wa mwaka kuliko ilivyo kuwa awali, nishati ya umeme hadi vijijini, huduma ya maji,kuongezeka kwa shule za msingi,sekondari na vyuo, viwanda vya mazao,mwamko mkubwa wa dhana ya ujasiriamali ndani ya jamii yetu,mitandao ya  mawasiliano, vyama vya kuweka na kukopa, kuongezeka kwa zahanati na vituo vya afya na uboreshaji wa hospitali ya mkoa wa Rukwa na za Wilaya.
Pia tumeweza kupata maeneo mapya ya kiutawala katika kusogeza karibu huduma za kijamii kwa wananchi hasa kuundwa kata mpya, tarafa, Wilaya, Halmashauri na mkoa. Hizi zote ni jitihada kubwa zilzofanywa na viongozi wetu hawa wa mwaka 2000-2015.
Mwaka 2000 tulikuwa na mkoa mmoja, Wilaya tatu na halamsahauri tano na leo tunazungumzia  mikoa miwili, Wilaya sita na halamsahauri tisa, awali hatukua na manispaa hata moja na sasa  tuna manispaa mbili (Manispaa ya Sumbawanga na Manispa ya Mpanda). Na pia kuna baadhi ya vijiji amavyo ni makao makuu ya tarafa vimepandishwa hadhi na kuwa miji midogo na makao makuu ya kila Wilaya yamepewa hadhi ya miji. Haya yote ni maendeleo na viashiria vyake. 

Kusukuma maendeleo ya kweli kunahitaji kujitolea kwa dhati na kujitoa mhanga.Kwa maendeleo haya machache tuliyoyataja na mengi ambayo hatutayataja kutokana na urefu wa orodha, yamewezekana na kuchangizwa kwa sehemu kubwa na nafasi na uzalendo wa ndugu yetu mpendwa mzee Mizengo Kayanza Peter Pinda hasa akiwa mbunge na waziri wa TAMISEMI na kisha akawa waziri mkuu wa Tanzania. Kwa uthubutu wake tuna mambo mahususi ambayo tuna kila sababu ya kutambua mchango wake binafsi na uunganishaji wake wa wabunge wa mikoa yetu uliotukuka na kumpa pongezi maalum. Baadhi ya mambo hayo machache ni kama: -
1.      Kusukuma na kutunisha mfuko wa Elimu mkoa wa Rukwa kwa kumbukumbu ya hayati Mwl. J. K. Nyerere ambao ulibuniwa mwaka 1999 na kuanza kutekeleza malengo yake  mwaka 2006 na mpaka unakabidhiwa rasmi kwa mkuu wa mkoa wa Rukwa mwaka 2010 ulikuwa umesaidia kupunguza tatizo la uhaba wa walimu kwa kuleta na kutoa motisha kwa walimu zaidi ya 800 wa diploma, Digrii na Crush programme kwaajili ya sekondari na chuo cha ualimu Sumbawanga, kusaidia kuanzisha shule sita za O’level (shule za sekondari Kalambo, Muze, Katuma, Rungwa, Ilemba na Usevya) na shule za A’level (Matai, Mambwe, Kizwite, Nkasi, Kate, Sumbawanga, Usevya na ) ambazo zisingeanza bila mfuko kudhamini wizarani kwa mfuko  kubeba jukumu la kutafuta walimu hitajika na wabunge wamajimbo husika kuchukua jukumu la kushawishi na kushrikiana na halamsahauri zao katika kujenga miundombinu hitajika na vifaa.
Mzee Pinda aliwezesha mfuko huo kufanya harambee kubwa hapa Dare s salaam chini ya ugeni rasmi wa Rais wa awamu ya nne.mh. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na kupata fedha zilizo saidia kuendelea kutafuta manesi, walimu na madaktari kwa ajili ya huduma ya afya na fedha zilizobaki ziliweza kutumika kuchangia ujenzi wa madarasa na hosteli za wasichana kwenye baadhi ya shule na nyingi zaidi ya milioni 250 zilinunua hisa/vipande kwenye mfuko wa umoja (UTT) na kwenye benki ya CRDB ili faida itakayo kuwa inapatikana itumike kusomesha watoto yatima na kudhamini watumishi kujiendeleza kitaaluma.Pia aliwezesha kupatikana mradi wa chuo cha VETA Mpanda.

Ndugu wanarukwa na wanakatavi
 Jitihada za mfuko huu zimewezesha kuutangaza vema mkoa wa Rukwa kwa wakati huo,kupanda kwa kiwango cha ufaulu, ongezeko la shule za kidato cha nne na cha sita. Miongoni mwa shule za kidato cha sita kati ya zilizoanzishwa kwa jitihada za mfuko iliweza kutoa mwanafunzi aliyefaulu vizuri na kuongoza kitaifa na shule yenyewe kushika nafasi nzuri kitaifa.
Kwa kuwa ni wazi kwamba ili wanadamu wamjue Mungu ni lazima wawe na Elimu ya kutosha, na kwakuwa mzee Pinda amesaidia jamii ya wanarukwa na Katavi kupata Elimu, hivyo basi mzee huyu tayari amepata thawabu kwa Mwenyezi Mungu maana amesaidia watu wake wamjue na kumtambua kupitia maandiko na upeo na uelewa waliopata.

2.      Jambo la pili kubwa alilofanya kwa uthubutu wake ni la kuanzisha mkoa mpya wa Katavi ambalo limeongeza na kusogeza fursa nyingi za kimaendeleo.Sasa tuna maeneo mengi mapya ya kiutawala ambayo yamesogeza karibu huduma za kiuchumi na kijamii na kuongeza nafasi na fursa za ajira kwa makundi mengi na kada mbali mbali kwenye mfumo rasmi na usio rasmi – maana miradi mingi imebuniwa na kuleta fedha.

3.      Jambo la tatu – ni kusukuma na kukamilika kwa Mradi wa miaka mingi wa barabara ya lami Sumbawanga – Tunduma na jitihada zake za kutafuta na kufanikisha Mradi wa barabara  za lami za Sumbawnaga- Mpanda na Sumbawanga – matai  - Kasanga na Matai-Kasesya japo hazijakamilika lakini walau kuna sehemu kubwa za kuonekana. Pia kuna barabara nyingi za changarawe zimepasuliwa na zingine kuboreshwa kwa viwango imara sana pamoja na madaraja muhimu. Kuna vijiji toka uhuru havikuwahi kuona “bus” hata kidogo(Kala na Wampembe) lakini hivi sasa wamesahau kabisa historia hiyo kutokana na uwingi wa vyombo vya usafiri vinavyo wafikia kutokana na uzuri wa barabara zilizi chongwa na kuwekewa utaratibu mzuri wa ukarabati.
Hii ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa uwanja wa ndege Mpanda na Sumbawanga.Hongera sana mzee Pinda.

4.      Jambo la nne-ameweza kusukuma miradi ya umeme kwenye eneo letu na kuwezesha baadhi ya maeneo yaanze kupata nishati husika na kusahau adha za huko nyuma.

5.      Jambo la tano-aliweka msukumo mpya mkubwa kwenye kilimo na matumizi ya powertiller na ufugaji wa nyuki, miradi ambayo imebeba taswira yake binafsi akiwa waziri mkuu, uzalishaji wa mazao umepanda sana ukilinganisha na huko nyuma.
Aidha naomba katamka  kwamba mzee huyu amesaidia sana mambo mengi(orodha ni ndefu sana) kupata msukumo wa utekelezaji ndani ya eneo letu la Rukwa na Katavi.Itoshe tu  kufahamika kwamba hakuna binadamu anayeweza yote na tena peke yake,na mkamilifu ni Mungu peke yake. Hivyo basi tunaomba kumpa pongezi maalum za dhati mzee wetu kwa utumishi wake wa kisiasa kwa kipindi chote na kustaafu salama nafasi ya uwaziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Uwaziri mkuu wake umetupatia sifa na heshima kubwa sana ndani na nje ya nchi, pale inapotafutwa Mh. Pinda anatoka wapi.
            Naomba kumaliza kwa kusema, mkuu wa wanasayansi na anga akiwa na wasaidizi   
            wake angani (astronomers) aliwaambia,”tambueni ya kwamba asiyejua aendako
             hawezi kupotea njia”.
“Viva mzee mizengo Pinda”
Ahsante sana.
Ndugu wasomaji,,kwa heshima na taadhima tunaomba,kwa niaba ya jumuiya hii upatapo ujumbe huu mfikishie  mzee Pinda hiki tulichomwandalia kwa ishara ya kutambua utumishi wake kwetu wana Rukwa na Katavi .

No comments:

Post a Comment

regnard